Mchoro huu umetengenezwa kwa kutumia Akili Bandia (AI). Unafikiriaje?
Methali yetu ya leo inasemwa pia kama:
Mtaka cha mvunguni sharti ainame
Methali hii hutumika kuwahimiza watu kufanya kazi kwa bidii na kujitahidi. Hatupaswi kutarajia kupata vitu tunavyotafuta isipokuwa tumekubali kuvitafuta katika mahali ambapo ni vigumu kupafikia.
Hapa kuna hadithi fupi inayoeleza methali hii, juu ya Mulla Nasreddin, mhusika mcheshi katika ngano za Kisufi.
Mulla [Nasreddin] alikuwa amepoteza pete yake sebuleni. Aliitafuta kwa muda, lakini kwa kuwa hakuipata, alitoka nje hadi uani na kuanza kuchungulia pale. Mkewe, ambaye aliona alichokifanya, akamwuliza: “Mulla, umepoteza pete yako sebuleni , kwa nini unaitafuta uani?” Mulla alishika ndevu zake akisema: “Chumbani kuna giza na sioni vizuri. Nilitoka nje kwenda uani ili kutafuta pete yangu kwa sababu kuna mwanga mwingi zaidi hapa.
- Usimulizi wa Houman Farzad. Imetafsiriwa kwa Kiingereza kutoka lugha ya Kiajemi na Diane L. Wilcox (1989), halafu nimeitafsiri kwa Kiswahili.
Kwa Kiingereza, kuna hadithi inayosimuliwa juu ya mlevi anayetafuta pesa (au funguo) karibu na taa. Hili ni toleo liliochapishwa katika gazeti ya Boston Herald (mwaka wa 1924):
[Afisa wa polisi alikutana na mwanamume akipapasa-papasa akipiga magoti] “Nilipoteza noti ya $2 kwenye barabara ya Atlantic,” kasema mwanamume huyo. "Nini kile?" aliuliza afisa aliyeshangaa. "Umepoteza notiya $2 kwenye barabara ya Atlantic? Kwa nini basi unaitafuta hapa Copley Square?" “Kwa sababu,” akasema akiendelea na utafutaji wake, “mwanga ni bora hapa."
Hadithi hii imekuja kujulikana kama "Streetlight effect" katika sayansi.
Asante kwa mshiriki mwenzetu kwa kupendekeza methali hii! Je, una methali ya kupendekeza? Shiriki hapa!