Mchapishaji Mkuki Na Nyota Publishers
Mateso, maumivu na siasa ni mambo yaliyojaa uchochezi mkali unaomsukuma mshairi kuzungumza waziwazi na kinagaubaga na hatimaye kumfanya mwandishi apandwe na jazba zinazofanya kazi fulani itoke nje ya kingo za ulingo wa kisanaa. Katika hali kama hii, mshairi lazima atunge wimbo unaoimbika ndani ya nafsi yake mwenyewe kwanza, wimbo utakaomwezesha kunyanyuka kitandani asubuhi huku akijua hayuko pweke, ana wenzake wenye maumivu kama au kuliko yake. Mohammed Khelef Ghassani ana weledi huu wa kubaki ndani ya kingo za ulingo wa kisanaa, weledi wa kuichenga siasa kwa namna ya kuipa nguvu kubwa zinazoficha na kuzimua unagaubaga na hata ukali wake.
Kuhusu Mwandishi
Mohammed Khelef Ghassani alizaliwa mwaka 1977 visiwani Zanzibar na ni mwandishi wa diwani kadhaa za ushairi, zikiwemo Andamo: Msafiri Safarini Siwachi Kusema: Uhuru U Kifungoni Kalamu ya Mapinduzi: Mapambano Yanaendelea na N’na Kwetu: Sauti ya Mgeni Ugenini, ambayo ndiyo iliyompatia tuzo ya Fasihi ya Kiafrika kwa Lugha ya Kiswahili iliyotolewa na Mabati-Cornell mwaka 2015. Mbali na kuwa mshairi, Mohammed Ghassani ni mwandishi wa habari anayeishi na kufanya kazi zake nchini Ujerumani.
...