Kitabu cha mbinu za ufundishaji na mkusanyiko wa mazoezi mbalimbali kwa ajili ya makocha na walimu wa somo la michezo.
Methodology handbook and compendium of exercises for coaches and Physcial Education teachers.
Mpendwa mwalimu,ukitaka kutumia michezo kama zana ya elimu kwa maendeleo na mabadiliko
katika jamii ni muhimu kuwa na watu wanoweza kupanga na kuandaa shughuli za michezo zenye
ubora. Unahitaji kufahamu jinsi ya kutumia vifaa na kujifunza michezo mbalimbali na sheria zake.
Hii ndiyo sababu iliyotufanya tuamue kuwafunza walimu wa somo la michezo katika ngazi ya chini.
Wewe ni mmoja wa walimu ambao wamepata mafunzo katika warsha ya siku tano juu ya kutumia
michezo ili kuboresha kujiamini kwa wanafunzi, kujenga umoja, kuboresha mawasiliano,
uwajibikaji na nidhamu. Mawazo yote yanayofundishwa katika yetu kwa walimu yanajumuishwa
katika kanuni hii: Michezo + Stadi Mabadiliko/Maendeleo
Kanuni hii ndio inayotuongoza katika malengo ya mradi huu wa michezo. Mradi huu haulengi
kuibua vipaji vipya au wanamichezo mahiri. Tunaamini kwamba michezo ni sehemu ya msingi ya
elimu. Tunaamini pia kuwa afya ya mwili hujenga afya ya akili. Hivyo shughuli za mradi huu pamoja
na mtaala wa warsha za walimu unaleta dhana mpya. Hatuhitaji kuona watoto wakikimbia kwa kasi
zaidi, wakiruka juu zaidi au kupiga mpira golini kama kipaumbele. Tunataka kuchangia katika
mabadiliko ya jamii, tunataka kusaidia kuleta maendeleo kwa kufundisha maadili kama vile
heshima, umoja, uwajibikaji pamoja na utatuzi wa matatizo kupitia michezo. Tunataka lengo kuu
liwe “maendeleo kupitia michezo” na si “maendeleo katika michezo”. Huu ni mtazamo mpya
unaolenga kuboresha maadili ya michezo maarufu kama vile soka, netiboli n.k. Lengo kuu si kuwa
na ushindani na kujipatia medali. Tunaamini kwamba si rahisi kuielewa falsafa hii tangu mwanzo
na ndio maana katika kitabu hiki cha walimu tunatoa ufafanuzi wa dhana hii na michezo ya stadi za
maisha inayofundishwa katika warsha.
...