Diwani ya Ustadh Andanenga imetumia vipengele vya mchomozo ambavyo ni takriri na ukengeushi. Kipengele cha takriri silabi / mizani ndicho kimejitokza zaidi. Diwani hii iliandikwa katika cha mwaka 1990, msanii akiwataka wananchi kufanya kazi na kujitegemea ili kuepuka kutegemea misaada kwa Wazungu. Diwani inawataka watu waishi kwa kupendana , wathamini lugha ya Kiswahili kwani huo ni ukombozi wa kifikra endapo tutathamini utamaduni wetu.
Mifano ya mashairi:
63. Fanya ulizio
1.
Leo ninajambo, nataka kwambia
Sikiza mrembo, badili tabia
Mapenzi ya shombo, sitavumilia
Nataka mapambo, sitaki udhia.
2.
Mapenzi ni ladha, iso mithilika
Hayana karadha, yataka hakika
Na kitu bughudha, penzi hufumuka
Hayataki adha, mapenzi ni shuka.
3.
Mapenzi ni dawa, ya watu wawili
Wagonjwa hupowa, wakawa sahali
Wakavuta hewa, hata ilo mbali
Kama hujajuwa, kaa ujadili.
4.
Na wala si haja, wengi kuambata
Mmoja ni tija, ni huyo limbata
Lumbata mmoja, pendo la mashata
Pendo la faraja, liwe la kumeta.
5.
Kama huyajui, fanya ulizio
Pendo makuri, halina shikio
Nasema sizui, naapa apio
Kama hutambui, uliza wenzio.
6.
Na hapa ni mwisho, shika yangu haya
Lisipate chosho, ukaja limwaya
Fanya linganisho, meno na mataya
Penzi suluhisho, katika kayaya.
64. Ai ghalibi ya ria
1.
Shairi lako shababi, somo bingwa wa utunzi
Nakiri yako kalibi, ya kwamba ukimfunzi
Akuzidishe Wahabi, umanju katika nyenzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
2.
Penzi kwa mtu ajabi, huhasimu wake wenzi
Akakana uswahibi, mfanyanayo hayafanzi
Akageuka usubi, akutobowe ja mwanzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
3.
Ukimwamba ya kitabi, ligaja lenu lijenzi
Hudhania wake bibi, unataka akuenzi
Atapandisha ghadhabi, akupakaze masinzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
4.
Huyakana matilabi, hukuletea magenzi
Mwambie ziba hazibi, uso akakunja sunzi
Hadi atokwe kidabi, akajuta kwa majonzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
5.
Hata aweke bawabi, na mabingwa wa ulinzi
Na waimbaji ayebi, nyimbo za Kongo za dansi
Asemapo audhnbi, amekwamisha kitanzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
6.
Wameshindwa matabibi, wa hilo hulifinyanzi
Waloweza kwa hesabi, kulipia bora kanzi
Walichovuna dhunubi, uhasama na simanzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
7.
Ziimarishwe nasabi, kama lombe na kigunzi
Kwa mshiko tabitabi, ja maua na kisonzi
Penzi lendapo gudubi, hakuna mshikwa ganzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
8.
Tamati ya kuratibi, penzi nyama ya mawinzi
Linapoza na kusibi, lina kiza lina lenzi
Kwa nguvu mtu hubebi, hufiki nalo Chamanzi
Ai ni sumu ya wenzi, penzi kwa mtu ajabi.
65. Pendo la pesa
1.
Pendo la pesa si pendo, mbali nalo jitengee
Pendo lanuka uvundo, mbali nalo lisogee
Pendo halina uhondo, katu usilichekee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
2.
Pendo halina utamu, lina harufu jamee
Pendo ninalilaumu, mimi lisinilemee
Pendo halina kudumu, hadi pesa umwekee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
3.
Pendo lataka kupenda, bila kupiga kengee
Pendo mfano wa tunda, ukila unenepee
Pendo la pesa huvyonda, tupa usilipokee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
4.
Pendo la kwa kila hali, ubora nalipotee
Pendo kutumia mali, ndipo aitike bee
Pendo hilo ni dhalili, mbali nalitokomee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
5.
Pendo kutumia hela, mifuko iteketee
Pendo hilo lahaula, ni zigo ujibebee,
Pendo wawili ni kula, nyama ndimi mnenee
Pendo alina sheree, pendo la pesa si pendo.
6.
Pendo kwa watu chaguo, lazima nielezee
Pendo ni sawa funguo, kufuli imngojee
Pendo la kupenda nguo, bora lichekwe heehee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
7.
Pendo ni la pale zama, wanahadithi wazee
Pendo lao likiuma, bila kusema nigee
Pendo sasa limelema, ukipanda lisimee
Pendo halina sherce, pendo la pesa si pendo.
8.
Pendo hapa nakomesha, mbele nisiendelee
Pendo la pesa lafisha, ni gonjwa usipokee
Pendo hadhi linafisha, la pesa sipendelee
Pendo halina sheree, pendo la pesa si pendo.
66. Kimada
1.
Bini Adamu amri, kamwe hazihifadhiki
Haziwekeki dahari, na kamwe hazilindiki
Kama vile za Kahari, ziloshushwa hazitoki
Kimada kakosa haki, kwani si ndoa kamili.
2.
Halingani na wa ndoa, kimada kakosa haki
Aweza kujiondoa, kama yeye hakutaki
Na mume kamchondoa, si shoti kumtaliki
Kkwani amekosa haki, sio wa ndoa kamili.
3.
Kwa kuwa kakosa hadhi, na ndipo hatamaniki
Muwekaji huwa radhi, watu wakimdhihaki
Kwa nakama na maudhi, bwana wake hashituki
Kwani kalemwa na haki, kakosa ndoa kamili.
4.
Sababu zake hususa, si radhi yake Maliki
Kuviweka vibubusa, kwa njia ya uzandiki
Jambo jema yatupasa, machafu kutoafiki
Na kimada hana haki, kama wa ndoa kamili.
5.
Umeoneka ukweli, mwezi juzi siyo wiki
Kimada kapewa feli, mbaya hazielezeki
Bwanawe akawa tuli, hakujali laizeki
Kimada kakosa haki, kwani si ndoa kamili.
6.
Ni maneno ya malenga, ya wapuzi siandiki
Maburudi na maanga, mazima hayatenguki
Bali kwa yule mjinga, atachimbia handaki
Kimada kakosa haki, kwani si ndoa kamili.
7.
Mfifi wa taadhima, yeye baya hatosheki
Huwenda nduu kugema, anywe tumbole husaki
Jaribu mwambie tema, atakukita mkuki
Na kimada hana haki, kwani si ndoa kamili.
8.
Na wenziwe mabwelele, manene ja pikipiki
Kapa ya masiku kale, ya leo hayaoneki
Hae! Najuta salale, kuwamo kindakindaki
Kimada kakosa haki, kwani si ndoa kamili.
9.
Ingawa kweli andiko, najuwa hatosadiki
Na pindi aje kwa foko, mwendo usio burcki
Asione ajabiko, kwa tungo akighariki
Mpinzi aonyesha haki, kwani si ndoa kamili.
...