Nyakati za mafanikio, watu wanapenda kuhusishwa na kudai pongezi, hata kama mchango wao ulikuwa mdogo. Lakini mambo yanapoharibika, watu wanakimbia na hulaumiana. Hii ndo maana ya methali "Ushindi una baba wengi, kushindwa ni yatima." (Success has many fathers, failure is an orphan.)
Kwa mfano, fikiria kama umepokea pesa za wawekezaji ili kuanzisha biashara. Biashara ikifanikiwa, wawekezaji wataiona kama mafanikio yao, wataiita "
biashara yetu", na itakuwa rahisi sana kutafuta wawekezaji wengi zaidi. Lakini ikiwa biashara imefeli, wawekezaji wako wataiita "
biashara yako" na kuomba urudishe pesa zao.
Mara nyingi unaweza kutambua kiongozi halisi wa biashara, shirika au kikundi kwa kuona ni nani anayewajibika nyakati za changamoto na matatizo. Kiongozi bora ni yule ambaye anashiriki sifa na pongezi na wenzake nyakati za kufanikiwa, na anakubali kuwajibika na kulaumiwa nyakati za kushindwa.
Methali hii ilitumika na Rais wa Marekani, John F. Kennedy, mwaka wa 1961, akiongea na waandishi wa habari baada ya mgogoro wa "Bay of Pigs". Lakini inaonekana kwamba chanzo halisi cha methali hii ni cha kale zaidi... inatoka Mwanahistoria wa Roma ya Kale aliyeitwa
Tasitus, katika
biografia ya jenerali Agrikola kilichoandikwa miaka 98 baada ya kuzaliwa Kristo, akieleza changamoto ambazo jeshi la Roma lilikabiliana nazo katika ukoloni wa Uingereza.
[Katika vita] sifa ya mafanikio hudaiwa na wote, wakati maafa yanahusishwa na mtu mmoja peke yake.
- Tacitus, Agricola
Je umewahi kuona mfano wa methali hii katika maisha yako? Tunaomba mawazo yako!