na Angelica A. 
Methali ya "mpanda ngazi hushuka" ina maana kwamba watu wanaopanda ngazi za mafanikio au mamlaka wanaweza kushuka haraka kutoka kwenye nafasi yao ya juu. Inatukumbusha kwamba hali ya mafanikio au umaarufu haijithibitishi kuwa ya kudumu au salama. Mambo yafuatayo yanathibitisha ukweli kuhusu methali hii;

 Hali ya Majivuno; Methali hii inaweza kutumika kuonyesha hatari ya kujivunia sana mafanikio au kuwa na kiburi. Inatuambia kwamba hali ya juu inaweza kubadilika ghafla, na mtu anaweza kupoteza kile alichokuwa nacho ikiwa hatakuwa makini au asipoweza kudumisha kiwango chake cha juu cha kazi au tabia nzuri.

 Kupandishwa cheo; Methali hii pia inaweza kutumika kuwahimiza watu wawe waangalifu na waangalie mbali zaidi, wasijiridhishe na mafanikio yaliyopatikana hadi wakati huo, na badala yake wajitahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kudumisha maadili yao ili kuepuka kuanguka. Methali hii inatufundisha baada ya kupandishwa cheo tusijisahau katika uwajibikaji wetu wa kila siku kwani kuna uwezekano pia wa kushushwa cheo au kupoteza cheo hicho tulichopata.

 Hali ya kuwa na Kiburi;  Katika maisha, methali hii  imekuwa ikitumiwa kwa muda mrefu sasa. "Mpanda ngazi hushuka." Methali hii inatufundisha somo muhimu kuhusu hatari ya kiburi na jinsi inavyoweza kusababisha kushuka kwa haraka kutoka kwenye nafasi ya juu. Hakika, methali hii ina umuhimu wake katika jamii yetu ya leo inatuhimiza tuwe watii kazini na kuwaheshimu wafanyakazi wenzetu. Katika jamii yetu ya leo, tunaona mifano mingi ya watu ambao wamepanda ngazi za mafanikio lakini wameanguka kutokana na kiburi chao. Kwa mfano, kuna watu maarufu na wenye mamlaka ambao wamejikuta katika matatizo makubwa baada ya kujisahau na kudharau wengine. Wamevurugwa na kiburi chao na wamesahau kuwa mafanikio yao yanategemea juhudi za wengine na msaada wa jamii yao. Kiburi kinaweza kusababisha mzunguko wa chuki na uhasama. Watu wenye kiburi hawataki kushirikiana na wengine au kusikiliza maoni na ushauri wanaopewa. Wanajiona kuwa juu ya wengine na hawana haja ya kujifunza au kuboresha. Kwa sababu hiyo, wao hujikuta wakitengwa na kupoteza ushirikiano na msaada wa watu wanaowazunguka.

Kupata Kazi; Watu wengi wanatafuta kazi kwa bidii ili wapate na baada ya kupata wanajisahau na kutowajibika wakiwa katika maeneo yao ya kazi na kusahau watu walio wasaidia wakati wanapotafuta kazi hali hiyo hupelekea wapoteze kazi walizo nazo na kufukuzwa kazini kama methali isemavyo "Mpanda ngazi hushuka" hivyo methali hii inahimiza watu wanapopata kazi wawe na heshima kwa jamii na wale wote walio wasaidia kupata kazi hiyo kwani wanapo kwenda kinyume na hivyo kunawapelekea kufukuzwa kazi na hali yao ya maisha kushuka  na kuwa katika hali ngumu ya maisha. 

 Hali nzuri ya kiuchumi;  Watu wenye uwezo mzuri wa kimaisha mara nyingi wanatumia hela na mali walizo nazo kwaajili ya kustarehe na kusahau kufanya vitu vya msingi kama kuwekeza hela walizo nazo kwenye biashara ili kupata faida zaidi na kuwadharau wengine wenye hali ya chini ya kimaisha. Wakati mwingine wanatumia hela walizo nazo kuponda raha kwa kuhonga na kuendekeza starehe  na kuwa na idadi ya wapenzi wengi wakiamini hela walizonazo zitawasaidia kupata watu wanao wahitaji matokeo yake wanaangukia kupata magonjwa ya zinaa. Matokeo yake baada ya kupata magonjwa wanaishia kujitibu magonjwa yasiyopona na kujikuta wanapoteza hela nyingi na kufilisika kila mara  wanabadilisha hospitali, wengine wanaenda kwa waganga wa kienyeji ili wapate dawa  za kuwatibu huku watu waliowathamini wakati wakiwa na afya njema wanawakimbia na kuhitaji msaada kutoka kwa wale waliowadharau wakati wakiwa na hali nzuri ya kiuchumi wakati mwanzoni waliwadharau na kuona hawana maana siyo hadhi yao. Methali hii ya  "Mpanda ngazi hushuka" inatufundisha tusiwadharau watu wengine hata kama tuna hali nzuri ya kiuchumi kwani ipo siku tajiri anaweza kufilisika na yule aliyedharauliwa maisha yake kubadilika na kuwa na hali nzuri kimaisha na kuwasaidia hata wale watu walikuwa wakimdharau kipindi hakiwa hana hali nzuri ya kimaisha.

Methali ya "mpanda ngazi hushuka" inahimiza watu kuwa waangalifu na waangalie mbali zaidi. Tunapaswa kudumisha unyenyekevu na kujifunza kutoka kwa wengine. Kupata mafanikio kunahitaji kazi kubwa, uvumilivu, na kujitolea.