We support Pickleball and Tennis in Arusha, Tanzania
Play tennis Learn more
Book a court Hire a tennis coach in Tanzania
Posts / Proverbs Proverb of the day
SW

Akiba Haiozi

na Rose Mwanri 🇹🇿 
🏆 Shindano la Insha ya Methali 
🥈 Mshindi wa Pili 

Akiba Haiozi

Methali ni usemi wa kimafumbo unaotumika katika jamii. Maneno katika methali huwa na maana ya ziada na methali huwa na pande mbili. Upande wa kwanza hutoa wazo na upande wa pili humalizia wazo. Akiba haiozi ni miongoni mwa methali za kiswahili inayotumika sana katika jamii za kiafrika na kwa watumiaji wa lugha ya kiswahili duniani, ikiwa na lengo la kuwaasa watu juu ya umuhimu wa kujiwekea akiba.

 Dhima ya methali hii ni kutusisitiza sisi wanajamii kujianda vema na maisha ya leo pamoja na kesho huku tukiwa tayari kuzikabili changamoto mbalimbali za maisha.

 Methali hii hutuonyesha ni kawaida mwanadamu kupatwa na dharura mbalimbali katika maisha ya kila siku. Mfano kupatwa na maradhi, ajali, au hata kifo. Pale unapokuwa na akiba uliyojiwekea itakusaidia wakati umepatwa na changamoto ya ghafla ambayo hukuitarajia.

 Faida nyingine ya kuweka akiba ni kuboresha maisha. Cha kwanza nashauri tuwe na utaratibu wa kuweka akiba mara kwa mara ili kuweza kuboresha maisha yetu kwa ujumla. Tunavyozidi kuweka akiba ndivyo ambavyo akiba hiyo inaweza kutusaidia kuboresha makazi yetu na miundombinu kwa ujumla ndani ya jamii zetu. Mfano mzuri ni wazazi ambao akiba wanazoziweka huwasaidia kulipa karo za shule pamoja na kununua vifa mbalimbali vya shulena hata gharama zingine zinazojitokeza kwa wakati huo.

 Methali hii pia inatukumbusha kuwa kadri tunavyozidi kuweka akiba ndivyo tunavyokuza hazina yetu. Swa na ile methali inayosema “ Haba na haba hujaza kibaba” ukichambua methali hizi zinaendana maana na utagundua ni ukumbusho mkubwa kwetu kuhusu ujenzi wa hatma njema ya jamii yetu ya sasa na baadae. Kwa kuwa zinatuhimiza kuwekeza kwa kila chumo tulipatalo. Tunakuza hazina kwa kuwa kile tunachoweka akiba kipo kwaajili yetu.

 Chukua nafasi kujiuliza, ni mara ngapi umepatwa na changamoto na akiba ndiyo ikaokoa jahazi, ni mambo mangapi yametokea bila taarifa na akiba ndiyo imetumika kuweka mambo sawa. Naamini sote tunapaswa kuweka akiba bila kujali kipato ni kikubwa au kidogo. Mfano unaweza kuanza kuweka akiba kidogo kidogo kutokana na kile unachokipata na kufikia muda Fulani utakuwa na akiba kubwa.

 Vilevile methali hii inasaidia kukuza maarifa kwa mtu mmoja mmoja na jamii hasa pale ambapo pamekuwepo na tofauti ya uhifadhi wa akiba kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Hapo zamani tunaambiwa watu walikuwa wanahifadhi akiba zao kwa kuchimba chini ya ardhi, kuweka chini ya kitanda au hata sehemu zingine ambazo wao waliamini ni salama. Leo hii watu hawatumii sana njia za kienyeji kuweka akiba zao. Ukija kwenye fedha zipo benki zenye mifumo thabiti na salama katika kuhifadhi fedha. Kwa upande wa akiba ya mazao pia zipo njia salama za kuhifadhi tena hata kwa muda mrefu bila kuharibika. Kwa hakika akiba haiozi.

 Waswahili tunasema “akiba haiozi”, “haba na haba hujaza kibaba” ikimaanisha kwamba akiba yaweza kuonekana ndogo ila kadri inavyoongezeka ndivyo inavyokuwa kubwa. Kinyume chake tunaambiwa “Chovya chovya humaliza buyu la asali”, “Bandu bandu humaliza gogo”. Tukikumbushwa kuwa vile tunavyochukua akiba zetu kidogo kidogo bila sababu ya msingi ndivyo ambavyo iko siku tutahamaki na kuona akiba imeisha bila kuona kitu cha maana kilichofanyika. Tukumbuke “mali bila daftari huisha bila habari”, tuangalie mfano wa shairi hili linalotusisitiza kuhusu kuweka akiba.

Akiba kweli hazina, haijawahi saliti,
Kwetu ni muhimu sana, hutubeba kwa nyakati,
Kipindi kweli hatuna, inasimama kwa dhati,
Sote tuweke akiba, akiba ni mkombozi.

 Kwa hakika ni dhahiri yatupasa kutunza vitu vyetu vizuri na rasilimali tulizonazo kwa kuweka akiba ili tuweze kujinusuru pale ambapo tunapokumbwa na changamoto za kushtukiza kwa ajili ya maisha yetu ya sasa na ya baadae.

Play Tennis or Pickleball in Arusha, Tanzania

Your reservations contribute to supporting:

for kids, teens and adults in Arusha, Tanzania

and the maintenance and upkeep of the courts.

We recently built 3 new lighted pickleball courts in Arusha, Tanzania!

Support fitness, sports and education in East Africa

Help us support great programs in East Africa