Publisher Chama cha Mapinduzi, Dodoma
Neno malezi au tendo la kumlea mtoto lina maana pana sana na kwa binadamu huanzia wakati wa mimba, kuzaliwa, utoto ,
ujana hadi utu uzima.
Kumlea mtoto kuna maana ya kumtoa gizani kusiko na uhakika wala usalama na kumwongoza mwangani kwenye uzoefu wa wahenga, wazazi na jamii. Kumlea mtoto vile vile kuna maana ya kumpa mahitaji ya lazima, kama vile chakula , mavazi, malazi na matibabu na kumpatia mahitaji ya burdani kama vile michezo na vifaa vya kuchezea. Kulea kuna maana ya kum tunza mtoto , kumhifadhi na kumkinga dhidi ya madhara, magonjwa na maadui ili apate kukua akiwa na afya njema ya mwili na akili na aliyetengemaa kwa maono.
Malezi pia yana maana ya kumwingiza mtoto katika jamii kwa kumfundisha maadili, mila na desturi za jamii , kumjengea fadhila na mwenendo mwema unaokubalika na jamii.
...